Monday, 17 April 2017

'Aqiyqah


 ‘Aqiyqah maana yake kilugha ni kukata, kwa maana ya kuchinja kwa sababu ni Sunnah inayohusu kuchinja. Na kisheria maana yake ni mbuzi anayechinjwa kwa ajili ya mtoto aliyezaliwa kama alivyofundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na ni muhimu kuzingatia sana kisheria, kwani lazima Sunnah hii ifanywe kama ilivyofundishwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na si vinginevyo.
 Kutoka kwa Anas amesema Mtume: “Kila mtoto amefungika na ‘Aqiyqah yake, itachinjwa kwa ajili yake siku ya saba na atapewa jina, na atanyolewa kichwa chake” (Ahmad na An-Nasaaiy).
Salmaan bin ‘Ammaar adh-Dhibbiy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mvulana ana ‘Aqiyqah, mtawanyieni damu na mumuondolee uchafu” (al-Bukhaariy).
 Kutoka kwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mvulana achinjiwe mbuzi wawili walio sawa, msichana achinjiwe mbuzi mmoja” (Ahmad na at-Tirmidhiy)
Hii ni Sunnah iliyokokotezwa, ikimaanisha ni Sunnah muhimu sana kwa aliye na uwezo kuifanya. Ni Sunnah kwa aliye na uwezo kwa sababu inahitajika kupatikana mbuzi au kondoo wawili kwa mtoto wa kiume na mmoja kwa mtoto wa kike, kutokana na Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hapo juu. Kwa sababu hiyo si wote waliopata watoto wanaweza kuitekeleza Sunnah hii, kwani inahitaji uwezo wa kununua wanyama hao. Kwa wasio kuwa na uwezo hawalazimiki kwao kuitekeleza Sunnah hii, kwa kufananisha Sunnah hii ni sawa na ibada ya Hijjah, inafanywa kwa walio na uwezo tu.
 Hivyo kitu cha kuzingatia ni kwa kwa wale walio na uwezo wa kupata mnyama ni muhimu sana kuifanya Sunnah hii, kwani ni Sunnah iliyosisitizwa. Ukiangalia kwa undani na uhaki si gharama kuifanya Sunnah hii hasa kwa wakati huu tulionao sasa hivi na pia kwa sisi tunaoishi mijini. Na cha kuzingatia zaidi ni kwamba tunafanya vitu vingine ambavyo havija thibiti katika mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na vingine ambavyo havipo katika mafundisho ya dini kabisa, wakati tunapojaaliwa kupata watoto, au watoto wetu wanapotimiza miaka fulani, kama Maulidi, baby showers na Birthday parties.
 Nini Cha Kufanya Anapozaliwa Mtoto Na Katika ‘Aqiyqah
Samurah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kila mvulana amewekwa rahani kwa ‘Aqiyqah yake achinjiwe siku yake ya saba, apewe jina siku hiyo na anyolewe kichwa chake” (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah).
  1. Kuchinja mbuzi wawili au mmoja kwa mtoto wa kiume au wa kike kama inavyofuatana. Kuna baadhi ya riwaya zinazosema mbuzi mmoja anatosha, lakini hazina nguvu, riwaya zilizokuwa na nguvu ni mbuzi wawili kwa mtoto wa kiume na mmoja kwa mtoto wa kike. Lakini inapotokezea kuwa Muislamu hana uwezo wa kuchinja mbuzi wawili basi mmoja pia inajuzu. Na mbuzi wawe ni wenye kusalimika na kasoro yoyote, na kwa watoto wa kiume mbuzi wawe ni wenye kufanana kimaumbile na kiumri.
  2. Kuchinja siku ya saba. Inapendeza zaidi kama ikiwezekana kuchinja siku ya saba, lakini kama itashindikana kotokana na udhuru usiozuilika basi bado inafaa kufanya baada ya siku ya saba.
  3. Kutoa jina kwa mtoto katika siku hii ya saba, na majina ni vizuri yawe majina mazuri kama tuliyofundishwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au majina ya Mitume, au ya Maswahaba, au ya watu wema waliotangulia.
  4. Kunyoa nywele na kuzipima kwa sonara na kutoa sadaka kiasi cha uzito wa nywele zilizokatwa, kwa thamani ya fedha.
  5. Inapendekezwa nyama hiyo igawanywe katika mafungu matatu; moja la watu wa nyumbani, jingine la masikini au wasiojiweza, na jingine la majirani na marafiki. Watu wakikutana na kula pamoja na kusherehekea neema hiyo ni jambo lenye kupendeza.
  6. Lingine la kukumbuka ni kumuadhinia mtoto anapozaliwa kwenye sikio lake la kuume tu kama walivyopendekeza wanachuoni ili neno la kwanza mtoto akalosikia ni neno la Tawhiyd. Kuhusu kumuadhinia na kumkimia kwenye sikio la kushoto, riwaya zake si sahihi.
  7. Na pia ni Sunnah kumlambisha mtoto anapozaliwa tende, asali au kitu chochote kitamu kitakachopatikana halali. Hakuna ushahidi wowote wa Hadiyth kuhusu mtoto kulambishwa kitu kichungu kama shubiri au chochote kwa madai kuwa mtoto anatakiwa aonjeshwe utamu na uchungu wa hii dunia! Hakika huu ni uzushi tu, na haijathibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) jambo hilo wala ufahamu huo. 
 Wanachuoni wamekhitilafiana na Sunnah hii ya ‘Aqiyqah na wamegawanyika katika makundi matatu na kila upande ukiwa na mtazamo wake tofauti.
Kuna wanaosema:
  1. Ni Sunnah na mustahabu (kinachopendeza). Na ushahidi wao umesisimama sana katika Hadiyth tulizozitaja hapo juu.
  2. Ni lazima na ni wajibu. Hoja yao ni Hadiyth ya Buraydah na Ishaaq bin Raahawayhi: “Hakika watu siku ya Qiyaamah watachunguzwa ‘Aqiyqah zao, kama watakavyochunguzwa Swalah zao”.
  3. Kukana uhalali wake, na wenye kauli hii ni wanazuoni wa kihanafi, na moja ya dalili zao ni Hadiyth ya ‘Amr bin Shu‘ayb amempokea babake kutoka kwa babu yake kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu ‘‘Aqiyqah, akasema: “Sipendi ‘Aqiyqah” (al-Bukhaariy). Lakini wamejibiwa kuwa Hadiyth hii si ya uhalali wa kupinga ‘Aqiyqah, bali ni kuonyesha tu kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakupendezewa na  jina hilo lenye maana ya kukata, na muelekeo wa Hadiyth unaonyesha kuwa ‘Aqiyqah ni Sunnah na mustahabu kama inavyojulikana kuwa Mtume mwenyewe aliwafanyia ‘Aqiyqah Hasan na Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhuma).
 Rai iliyokubalika na iliyo na nguvu ni kuwa ‘Aqiyqah ni Sunnah Muakkadah kwa wanachuoni wengi, maimamu na wenye elimu. Basi ni juu ya wazazi wanapojaaliwa mtoto na wakawa na uwezo wa kuifufua Sunnah hii ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) afanye hivyo ili apate fadhila na ujira utokao kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala), na pia ili azidishe utangamano, mapenzi na mafungamano katika jamii.
 Umuhimu Wa Sunnah Na Kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)
Wengi katika Waislamu tunalifahamu neno “SUNNAH” kinyume na maana yake, kwamba ni kitu cha khiyari kufanya kama utapenda na utapata thawabu kukifanya na hutopata dhambi ukikiacha. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
“…Chochote atakachokupeni Mtume, kichukueni, na chochote alichokikataza kiacheni, na muogopeni Allaah kwani Allaah ni Mkali katika kuadhibu.” Al-Hashr: 7.
Maana ya Aayah hii ni kwamba ni waajib kwa kila Muislamu kuishi maisha yake yote kama alivyoishi na kufundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na hii ni AMRI kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), kwamba tumtii Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kumtii ni kufuata yale tu aliyotufundisha. Kwa maelezo ya Aayah hii Sunnah ni mwenendo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambao tumeamrishwa tuufuate, na si tuendeshe maisha yetu kwa jinsi tunavyofikiria sisi.
Pia amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika Aayah nyingine:
“Sema (Ee Muhammad) (kwa binaadamu): kama kweli mnampenda Allaah basi nifuateni mimi (Sunnah zangu). Na Allaah atawapenda nyie na atawasamehe makosa yenu, na Allaah ni mwenye kusamehe na mwenye huruma:” Al-‘Imraan: 31.
Bila shaka hakuna Muislamu yeyote ambaye hataki kupendwa na Allaah, Basi kama jibu tunapenda ni wajibu wetu kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ndipo Allaah Atatupenda. Na kama hatutompenda Mtume (Sunnah) basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Hatotupenda na wala Hatotusamehe makosa yetu.
Kama tunavyojua kuwa nguzo ya kwanza ya Uislamu ni Shahada, na shahada ni kukubali kikweli kabisa kisiri na kidhahiri kuwa hapana mola wa haki anayepasa kuabudiwa ila Allaah na Muhammad ni mjumbe Wake, basi ni wajibu wetu kufuata Sunnah za Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili tuwe tumeingia katika kuikubali hiyo nguzo ya shahada kikwelikweli.
Ni muhimu sana kwa Waislamu kufahamu kwamba huu ndio muongozo kwa kila tunachofanya na hatokuwa mtu Muislamu mpaka atekeleze kivitendo maneno haya mawili, na kutekeleza kwake ni kufuata Qur-aan na Sunnah, kwa maana kutotekeleza kivitendo maneno haya mawili ni sawa na kuubomoa Uislamu, maana hauwezi kusimama bila ya nguzo hii muhimu sana ya kwanza. Na kauli hizi mbili (Shahada mbili) zinakwenda pamoja na ni lazima zitekelezwe pamoja, na kwa Muislamu kuacha au kutofuata Sunnah, ni sawa na kutotekeleza nguzo hii muhimu.
Pia katika nguzo sita za Iymaan, nguzo ya tatu ni kuamini Mitume wote wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), si kwa kuwajua majina na idadi yao tu, bali kukubali waliyoteremshiwa na kutekeleza kivitendo waliyoamrisha na kuyaacha waliyokataza, kwa maana ya kwamba Muislamu yeyote kutokuamini nguzo hii ni sawa na kukosa Iymaan, na sijui utakuwa ni Muislamu wa aina gani bila ya Iymaan.
Umuhimu wa kufuata Sunnah si kwa baadhi ya Ibada tu na Sunnah iliyotajwa hapo juu, bali ni kwa Sunnah zote kama alivyofundisha mwenyewe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kufanya kinyume au kufanya kisichofundishwa na Mtume si vibaya tu bali ni dhambi.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika Qur-aan:
“Sema: Je, tukutajieni wenye khasara mno katika vitendo vyao?

Ni wale ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kwamba wanafanya kazi nzuri.

Hao ni wale waliozikanusha Ishara za Mola wao Mlezi na kukutana naye. Kwa hivyo vitendo vyao vimepotea bure, na wala Siku ya Qiyaama hatutawathamini kitu.

Hiyo Jahannamu ni malipo yao kwa walivyo kufuru na wakafanyia kejeli Ishara zangu na Mitume Wangu.” Al-Kahf: 103-106

Maana ya Aayah hizi ni kwamba kutenda matendo kwa kufikiria kwamba tutapata thawabu kuna hatari kubwa vitendo hivyo vikaathiri mizani zetu siku ya malipo na tukajuta kwa yale ambayo tumeyafanya (Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atunusuru tusiwe wale wenye kujutia tulio yafanya.) Na katika aya ya 106 inaonyesha hatari ya kumfayia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) dhihaka kwani malipo yake ni adhabu kali ya moto.
Katika mafundisho ya dini kukubalika kwa matendo mazuri ni lazima masharti mawili yafuatayo yakamilike:
  1. Nia ni lazima iwe ni kufanya kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wataala) peke yake, na si kujionyesha au kupata sifa au kupata kitu kingine chochote.
  2. Matendo ni lazima (waajib) yafanyike kama alivyofundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndio muongozo wetu wa matendo yetu ya kila siku.

Imepokewa na mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mtu yeyote atakayezua jambo ambalo halipo kwenye dini yetu, basi jambo hilo litakuwa ni lenye kurudishwa” Al-Bukhaariy
Kutokana na mafundisho tunayoyapata katika Aayah na Hadiyth zilizotangulia ni kwamba ili Muislamu aweze kuishi kama Muislamu ni lazima atekeleze maamrisho ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kama alivyofundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na si vinginevyo. Na ili tuyafahamu mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni lazima tujifunze (kutafuta elimu) na tusitegemee kusikia na kufanya mazungumzo ya kawaida ndio tutafahamu. Si vibaya kukaa na kuzungumza masuala ya Dini, ni vizuri na bora kuliko kupiga porojo, lakini tusitegemee kuwa ndio yatakuwa mafundisho tosha katika kufahamu dini yetu, inatubidi tutafute elimu kwa jitihada za kutafuta kwa nia ya kufahamu mafundisho ya dini yetu.
Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa sasa hivi kuna njia nyingi sana za kuweza kupata Elimu, lakini cha kuzingatia ni kwamba tuhakikishe Elimu tunazozitafuta ni sahihi kwani zikiwa ni uzushi basi zitakuwa ni zenye kukataliwa na kurudishwa kama Hadiyth iliyotangulia hapo juu iliyopokelewa na mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) inavyotufundisha. Hatutakuwa na udhuru wowote wa kusema kwamba hatukujua yalio sahihi, kwani kila kitu kipo wazi na elimu inapatikana kwa jitihada za kila mtu.
Imekusanywa na Ramadhaan Burhaan 

No comments:

Post a Comment