Kwa
jina la Allaah, Mwingi wa Rehma, Mwenye Kurehemu.
Sehemu
Ya Kwanza
Katika
usiku wa giza, Abu Lu’lu’ Al-Majuusi alijificha katika vivuli akijiandaa kwa
ajili ya Swalaah ya Alfajiri, wakati ambapo ataendesha mipango yake ya
kishetani kumuua Amiyr wa waumini – ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allahu
‘anhu).
‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) alikuwa (na kawaida) ya kuongoza Swalah ya
Alfajiri huku akisoma surah ndefu, akiwapa wafuasi wa jamii, muda wa kuhudhuria
mkusanyiko (wa Swalaah). Katika siku hii, wakati (‘Umar) akisoma (Qur-aan),
Abuu Lu’Lu’ akachukua hatua kutoka kwenye nguzo inayofifia, hali ya kuwa ana
kisu cha sumu katika mkono wa vazi lake. Akaruka mbele ya ‘Umar (Radhiya Allahu
‘anhu) na akamkata tumbo wazi kwa (kile) kisu. Baada ya hapo, akajaribu
kuukimbia mkusanyiko. Akiwa ana chana chana mbele na nyuma, akiwauwa watu wengi
zaidi ambao walikuwepo katika njia yake. Swahaabah mmoja akamtupia nguo juu
yake na alipo tahayari kwamba keshakamatwa Abu Lu’lu’ akajiua.
‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (Radhiya Allahu ‘anhu) akaikamilisha Swalaah ya
Alfajiri ambayo aliianza ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu). ‘Umar (Radhiya Allahu
‘anhu) alikamilisha Swalaah yake hali ya kuwa ni miongoni mwa watu (maamuma)
katika Jama’ah na akafariki dunia baadaye katika kitanda chake, (Radhiya
Allaahu ‘anhu).
Umuhimu wa Swalaah katika Uislamu hauwezi kudharauliwa. Ni nguzo ya
kwanza ya Uislamu iliyotajwa na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) baada ya tamko la Imani (shahaadah), ambayo kutokana nayo mtu
huwa Muislamu.
Swalaah imefaradhishwa kwa Manabii na watu wote. Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala) Alitangaza hadhi yake ya kuwa ni faradhi katika tukio Tukufu. Kwa
mfano, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alipozungumza na Muusa (‘Alayhis Salaam),
Amesema:
{{Nami nimekuteua wewe; basi sikiliza unayofunuliwa. Hakika Mimi ndiye
Mwenyezi Mungu. Hapana mungu ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na ushike Swalah
kwa ajili ya kunikumbuka Mimi}} [Twaaha: 13-14]
Hivyo hivyo, Swalaah imefaradhishwa kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati alipopelekwa mbinguni. Zaidi, wakati Allaah
(Subhaanahu wa Ta’ala) Anawasifu waumini kama katika Suratul-Al-Mu-uminuun,
moja katika sifa ambazo Anazitaja kuhusiana nao ni kule kushikana kwao na
Swalaah:
{{Hakika wamefanikiwa Waumini. Ambao ni
wanyenyekevu katika Swalah zao}} [Al-Mu’minuun:
1-2]
Umuhimu wa Swalaah unaendelea kuonyeshwa katika kauli nyingi za Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa mfano, Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:
“Jambo la kwanza ambalo mja atahukumiwa katika Siku
ya Hisabu ni Swalaah. Kama ikiwa ni nzuri basi amali zake zilizobakia zitakuwa
nzuri. Na ikiwa ni mbaya, basi amali zake zilizobakia zitakuwa mbaya.” [At-Twabaraaniy].
Kwa kweli, ikiwa Swalaah imeswaliwa vizuri
ikiambatana na ukumbusho wa kweli wa
kumkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), na kumgeukia Yeye kutaka msamaha,
itakuwa na athari kubwa juu ya mtu kwa kipindi
kirefu. Mtu anapokamilisha Swalaah yake, moyo wake utajaa ukumbusho wa
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Atakuwa ana hofu na pia vilevile matarajio juu
ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Baada ya tukio hilo, hatotaka tena kuondoka
kutoka katika sehemu hiyo ya fakhari kuelekea kwa ile ambayo ndani yake
atamuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) anaitaja
hali hii ya Swalaah katika Qur-aan:
{{Hakika Swalah inazuilia mambo machafu na maovu}} [Al-‘Ankabuut: 45].
Lakini
katika wale ambao wanaoswali, utakuta kuna vitendo vya kivivu ambavyo vinahitaji
kumulikwa. Kwa mfano:
· Wengine hawazingatii kile ambacho wanakisema.
· Wengine wanafanya haraka katika Swalah zao
· Wengine wanaachilia nadhari yao ya macho
izurure wakati wa Swalah
· Wengine mara kwa mara husahau nambari ya
rakaa zilizotimizwa.
· Dunia inakumbatia mioyo ya baadhi ya watu
wakati wa Swalah na inafunika akili zao.
· Na watu wengine katika Jama’ah wanaanza
kusujudu kabla hata ya Imaam kusema “Allaahu Akbar”
Linganisha hii (hali yetu katika Swalaah) na
Swalaah za watu ambao walikuja kabla yetu. Watu walikuwa wanafikiria ya kwamba
Ar-Rabiy’ bin Khaytham alikuwa ni kipofu kwa sababu ya kuinamisha macho yake
mara kwa mara. Alikuwa akiishi nyumbani kwa AbduLlaah bin Mas’uud (Radhiya
Allahu ‘anhu) kwa miaka ishirini na mtumwa wake wa kike akimuona alikuwa
akisema: “Rafiki yako kipofu anakuja” na AbduLlaah alikuwa akimcheka kwa kauli
yake.
Ndani ya AL-Bukhaariy na Muslim, Abuu Hurayrah (Radhiya
Allahu ‘anhu) anatueleza ya kwamba, kuna mtu aliingia msikitini, ambao Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) alikuwa amekaa.
Akaswali rakaa mbili na kisha akaja kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akatoa salamu. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) akaijibu salamu
yake na halafu akasema, “Rudi tena ukaswali kwani hukuswali.” Hivyo, yule mtu
akarudi, akaswali (rakaa mbili) kama alivyofanya mara ya kwanza, akaja tena na
kurudia kutoa salamu. Mtume Muhammad (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaijibu
salamu na akasema “Rudi tena ukaswali kwani hukuswali.” Hivyo, yule mtu akarudi, akaswali (rakaa mbili) kama alivyofanya mara
ya kwanza akaja tena na kurudia kutoa salamu. Mtume Muhammad
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijibu salamu kwa mara nyingine tena na kwa mara nyingine tena akasema:
“Rudi tena ukaswali kwani hukuswali”. Hadi
kufikia mara hii ya tatu, mtu huyo alisema: “Naapa kwa Yule ambaye alikutuma wewe na ukweli, Ewe Mtume wa Allaah,
sijui vyovyote isipokuwa hivi, Nifundishe.” Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
“Ikiwa unasimama kwa ajili ya Swalaah sema
“Allaahu Akbar”. Halafu soma ambacho kitakujia kwa wepesi katika Qur-aan. Kisha
rukuu mpaka utakapohisi kwamba umetulia katika rukuu yako. Kisha, simama mpaka
uwe umesimama wima kisawa sawa. Kisha, sujudu mpaka uwe umetulia katika sujudu
yako. Kisha keti mpaka uwe umetulia katika juluus yako. Kisha sujudu mpaka uwe
umetulia katika sujudu yako. Na uwe unafanya hivi ndani ya Swalaah yako yote”.
(Kwahiyo turudi tukarudie Swalah zetu)
Kwanini tunakuja msikitini; nini sababu yetu
ya kutekeleza Swalah? Tunafanya hivyo kwa kufuata amri ya Muumba wetu
(Subhaanahu wa Ta’ala). Kwanini hasa tupoteze baraka na thawabu kwa sababu ya
moyo usiotulia na mkono unaowasha. Khushuu ni kiini cha Swalaah zetu. Khushuu
ni matunda ya imani yetu. Lakini, hata baada ya kujua haya, watu hawafanyi
juhudi kukamilisha Swalah zao na kwa hiyo huandikiwa sehemu ndogo tu. Mtume
Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema;
“Kwa hakika, mtu ataondoka (katika Swalaah yake) na
ataandikiwa (thawabu) kumi za Swalaah yake; tisa, nane, saba, sita, tano, nne,
tatu, nusu.” [Abu Daawuud na at-Tirmidhiy]
‘Uthmaan bin Abii Dahshah (Radhiya Allahu ‘anhu)
alisema: “Sijawahi
kuswali Swalah ambayo baada yake nilikosa kumuomba Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala) Anisamehe kwa upungufu wangu katika Swalah ile.”
Mtu ambaye anaharakisha Swalah yake ni mwizi. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) alisema katika Hadiyth sahihi, “Mwizi muovu kuliko wote ni yule ambaye anaiba katika
Swalaah yake”. Swahaaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakauliza: “Ewe Mjumbe wa Allaah, anaibaje katika
Swalah yake?” Naye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hakamilishi rukuu na sujudu
zake”
Kwa sababu ya kasi ya jinsi ya watu
wanavyoswali, wanaonekana kama ndege, wanaodonoa juu na chini. Mtume Muhammad
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza mtu kudonoa (katika Swalah) kama kunguru.
‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) wakati mmoja alisimama katika Minbari
akiuhutubia umati wa watu kwa sauti ya nguvu akisema, “Mtu anaweza akakulia mpaka utu uzima katika Uislamu na asiweze kamwe
kukamilisha kwa ajili ya Allaah hata Swalah moja!” (Watu) wakasema, “Vipi hali
hii?” (‘Umar) (Radhiya Allahu ‘anhu) akasema: “Hakamilishi khushuu yake, hata
unyenyekevu wake, hata nadhari yake juu ya Allaah ‘Azza wa Jalla.”
Wakati mmoja, Ma’aruuf Al-Karkhiy (Rahimahu Allaah)
aliposimama miongoni mwa wanafunzi wake, mmoja wao akamwambia mwenziwe, “Tafadhali swalisha Swalaah
ya ‘Ishaa”. Mwanafunzi wa kwanza akakubali lakini akasema “Nitaswalisha Swalaah ya ‘Ishaa kwa sharti ya kwamba wewe
utaswalisha Swalaah ya Alfajiri sio mie” Ma’aruuf Al-Karkhiy alishtushwa
na kauli aliyoisema na akasema, “Naapa kwa Allaah,
ikiwa unafikiria ya kwamba utakuwa hai wakati wa Alfajiri, basi naapa kwa
Allaah, hujakamilisha Swalah yako”.
Sehemu Ya Pili
Jinsi ya kuwa na Khushuu ndani ya Swalah
Al-Qaasim bin Muhammad (Rahimahu Allaah) alisema: “Nilikwenda nje siku moja, na kila
nilipotoka ni lazima nipite kwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anha) na
kumsalimia. Siku hiyo nilitoka na nilipomkuta mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anha)
akiswali Swalah ya Dhuhaa, akisoma tena na tena Aayah ya Allaah:
{{Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa
(adhabu ya Allaah). Basi Mwenyezi Mungu Akatufanyia hisani na Akatulinda na
adhabu ya Moto.}} [At-Twuur: 26-27]
Alikuwa analia na akimwomba Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala) na huku akirudia Aayah hiyo. Nilisimama pale mpaka nikachoka, hali ya
kuwa yeye amebaki kama nilivyomkuta. Nilipoona haya nilijiambia, “Hebu niende
sokoni, nifanye ninachotakiwa kufanya, halafu nije tena”. Kwa hiyo, baada ya
kumaliza kufanya nilichotaka kufanya sokoni, nilirudi kwa mama wa Waumini
‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anha). Alikuwa kama nilivyomuacha, akirudia Ayaah,
akimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na akilia”.
Vipi tuwe na khushuu katika Swalaah?
Katika Sunnah ya Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam tunafundishwa yafuatayo:
1. Njoo mapema kwa ajili
ya Swalaah na jitayarishe kuwa na khushuu.
Fuatiliza adhana pamoja na
Mu’adhin na baada ya adhana, sema dua iliyoamriwa. Omba dua baina ya Adhaana na
Iqaamah. Tia wudhuu vizuri, hali ukisukutuwa mdomo wako, na vaa nguo zako nzuri
kabisa.
2. Nuia kupata dhawabu
zote za Swalaah yako.
Abu Bakr bin ‘Iyaash
alisema, “Nilimuona
Habiyb bin Thaabit katika sujudu. Ukimuona utadhania kwamba kashakufa (kwa
urefu wa sujudu zake).”
3.
Zingatia Aayah na adhkaar ambayo inasomwa ndani ya
Swalaah.
Fikiria kuhusu maana za Aayah ambazo unazisoma. Je haivunji moyo ya kwamba mtu
anaweza kuswali miaka kumi baada ya kumi, siku baada ya siku na pia bado hajui
anasema nini? Qur-aan iliteremshwa ili itafakariwe! Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala) Kateremsha (katika Qur-aan Ayaah inayosema):
{{Na hiki Kitabu,
Tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike
wenye akili.}} [Swaad: 29].
4. Swali Jama’ah. Allaah
(Subhaanahu wa Ta’ala) Anaamrisha:
{{Na shikeni
Swalah, na toeni Zakaah, na rukuuni pamoja na wenye kurukuu.}} [Al-Baqarah: 43].
5.
Usikose kamwe kuswali Swalah zako za nawaafil
(Sunnah zilizotiliwa mkazo), hasa zile ambazo Mtume Muhammad (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali siku zote, kama vile Witri na
Sunnah ya Alfajiri.
6. Usiharakishe Swalah yako.
Chukua muda wako na
usikubali kuifanya Swalah yako kuwa kitendo kilichokuwa hakina thamani katika
siku yako. Ibn Wahb (Rahimahu Allaah) alisema: “Nilimuona
Ath-Thawriy (Rahimahu Allaah) kwenye Kaa’bah.
Baada ya Swalah ya Magharibi, alinyanyuka kuswali na kisha akasujudu.
Hakunyanyuka katika ile sujudu mpaka adhana ya ‘Ishaa ilipoadhiniwa.”
7.
Jua ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anajibu
Swalah yako. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
alisema:
“Allaah
(Subhaanahu wa Ta’ala) Aliyetukuka alisema: “Nimeigawa Swalah kati Yangu na mja
Wangu katika nusu mbili, na mja Wangu
atapata alichokiomba” [Kutoka katika Surat ul- Faatiha ] Wakati mja anaposema,
“Sifa njema zote ni za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), Mola Mlezi wa viumbe
vyote,” Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema, “Mja Wangu Amenihimidi” . Wakati
mja anaposema “Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.” Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala) Anasema, “Mja wangu Amenisifu.” Wakati mja anaposema, “Mwenye Kumiliki
Siku ya Malipo”, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema mja Wangu
Amenitukuza”. Wakati mja anaposema, “Wewe tu tunakuabudu na wewe tu tunakuomba
msaada.” Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) anasema, Hii ni kati Yangu Mimi na mja
Wangu, na mja Wangu atapata alichokiomba”. Wakati mja anaposema “Tuongoze
katika njia iliyonyooka, njia ya
uliowaneemesha, sio ya wale uliowakasirikia, wala ya wale waliopotea,”
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema,
“Hivi vyote ni kwa ajili ya mja Wangu, na mja Wangu atapata alichokiomba” [Muslim]
8.
Swali pamoja na kizuizi (weka sutrah) mbele yako na
swali karibu yake.
Kitu chengine ambacho
kitakusaidia kuwa na khushuu’ [utulivu] ni kushughulika (au kuwa makini) katika
suala la kuwa na kizuizi (sutrah) na kuswali karibu yake. Kuwa na sutrah
kutazuia uoni wako, kutakulinda juu ya Shaytwaan, na kutazuia watu kupita mbele
yako, kitu ambacho husababisha wasiwasi na hupunguza thawabu za Swalah. Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
“Ikiwa mmoja
wenu ataswali basi na aswali akielekea kwenye sutrah, na awe karibu nayo” [Abuu Daawuud].
9. Tafuta ulinzi] kwa
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kutokana na Shaytwaan.
Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitufundisha vipi tupambane na wasi wasi wa
Shaytwaan. Abu’l- ‘Aas (Radhiya Allahu ‘anhu)
kasimulia ya kwamba alisema, “Ewe Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam), Shaytwaan ananisumbua wakati ninaswali, na hupata wasiwasi katika
kisomo changu.” Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
akasema, “Huyo ni Shaytwaan ambaye jina
lake ni Khanzab. Ikiwa utahisi kwamba yupo, jilinde kwa Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala) kutokana naye, na tema mate (makavu) katika upande wako wa kushoto mara
tatu”. Abu’l –‘Aas (Radhiya Allahu ‘anhu) alisema: “nilifanya hivyo na Allaah
(Subhaanahu wa Ta’ala) Akaniondoshea.” [Muslim].
10. Swali kama kwamba umeambiwa kuwa baada kumaliza Swalah utarudi kwa
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Abu Bakr Al-Muzaniy (Subhaanahu wa Ta’ala), alisema, “Kama
unataka Swalah yako ikufae, basi sema: “Nitakufa baada tu ya Swalah hii!”
Imeandikwa na
Muhammad Ash-Shariyf
Imefasiriwa
na Ilyaasa Mawlaana
No comments:
Post a Comment